Share news tips with us here at Hivisasa

Huku asilimia kubwa ya kaunti nchini zikiwa bado chini katika masuala ya maendeleo, spika wa bunge la Seneti Ekwe Ethuro amependekeza kaunti zilizo na viwango vya juu vya umaskini kupata mgao wa juu wa pesa maendeleo ya kaunti.

Bwana Ethuro amesema kuwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa kaunti husika kuafikia malengo yao na kuziba pengo lililoko baina ya kaunti ambazo zimeendelea tayari kama vile Nairobi na Mombasa.

Kwenye kikao kilichowaleta pamoja maseneta kutoka kaunti zote nchi mjini Mombasa mwishoni mwa wiki, Ijumaa, baina ya Seneti na kamati maalum inayoshughulikia masuala ya mgao wa fedha za serikali za kaunti, CRA, spika Ethuro aliwataka viongozi waliofumana kwenye mkutano huo kuwa na msimamo mmoja ili kufanikisha azimio la ugatuzi.

Spika Ethuro alisema kuwa dhamira kuu ya Seneti na shabaha halisi ya serikaki kugatuliwa ni kufanikisha luwaza ya mwaka wa 2030 na kutimiza malengo ya milenia kwa kusawazisha ukuaji wa uchumi kwa kila eneo nchini hasa yale maeneo ambayo yameachwa nyuma kwa mujibu wa historia.

"Kupitia uwezo tuliopewa kwenye katiba tuna nafasi ya kufanikisha malengo ya ugatuzi na tukiwa na msimamo mmoja tutafaulisha malengo hayo," aliongeza Ethuro.

Bwana Ethuro ambaye pia anatoka katika maeneo ya Kaskazini mwa Kenya ambapo nyingi ya kaunti za maeneo hayo yamekuwa nyuma kwa maendelea kwa muda mrefu alipendekeza kila kiongozi alionyesha mwelekeo na kuunga mkono dhamira hiyo.