Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Licha ya sekta ya afya kugatuliwa, fedha zinazosambazwa mashinani ili kuisimamia sekta hiyo ni chache mno kinyume na wakazi walivyotarajia kufaidika na sekta hiyo.

Akiongea katika eneo la Mariakani mjini Mombasa siku ya Ijumaa baada ya kuzinduliwa kwa kwa kituo kipya cha uchunguzi wa kiafya, Gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Jeffa Kingi alisema kwamba fedha nyingi zimesalia kwenye serikali kuu, huku serikali za kaunti zikihangaika pakubwa katika kukabiliana na changamoto nyingi za kiafya.

Kingi aliongezea kwamba kinyume na inavyopendekeza katiba kuhusiana na swala la ugatuzi, majukumu mengi kuhusiana na sekta hiyo ya afya yamekabidhiwa serikali za kaunti, ugavi wa fedha ili kuidhibiti sekta hiyo ingali changamoto kubwa na akaishinikiza serikali kuu kutathmini upya namna ya kuiimarisha sekta hiyo.

“Sekta ya afya mashinani inakumbwa na changamoto nyingi sana hata baada ya kugatuliwa, na hili limechangiwa na serikali kuu kutotutengea fedha za kutosha na kutulazimu sisi kama viongozi kutafuta kila namna ya kukabiliana na changamoto nyingi za kiafaya,” alisema Gavana Kingi.

Gavana Kingi alimtaka Waziri wa afya James Macharia kukutana na Viongozi wa kaunti ili kujadiliana kuhusu jinsi sekta hiyo ya afya itakavyoimarishwa na wakaazi mashinani kupata huduma za kisasa za matibabu.

“Tunamtaka Waziri wa Afya nchini James Macharia kujitokeza waziwazi na kuweka vikao vya majadiliano ili nasi kumueleza changamoto tunazozipita huku mashinani katika sekta ya afya na ikiwezekana basi atuongezee fedha zaidi katika sekta ya afya ili wananchi wetu wapate huduma bora za kiafya,” aliongeza Kingi.