Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua amekanusha madai kwamba wagonjwa wanauziwa damu katika Hospitali ya Mkoa mjini Nakuru.

Akiangazia taarifa iliyokuwa kwenye gazeti moja la humu nchini, Gavana Mbugua alisema kwamba alisikitika kusoma taarifa hiyo.

Akizungumza kwenye hafla ya maombi ya kwanza ya kaunti yaliyofanyika siku ya Ijumaa katika uwanja wa mkahawa wa Rify Valley Sports Club Nakuru, Gavana Mbugua alisema hakuna damu yoyote inayouzwa kwenye hospitali yoyote katika Kaunti ya Nakuru.

“Nilipokuwa nikisoma gazeti kwenye gari, niliona taarifa kuwa damu inauzwa katika hospitali zetu na nikashtuka sana kwani damu ni uhai. Nilikuwa mwenye hofu sana niliposikia hivyo. Hata hivyo, ninaweza kuwahakikishia kuwa madai hayo si ya kweli,” alisema Mbugua.

Kwa muujibu wake, taarifa hiyo ilizuka kutoka kwa mmoja wa wanahabari aliyetofautiana na meneja anayesimamia benki ya damu, hatua iliyompelekea kuchapisha taarifa hiyo.

Mbugua alisisitiza kwamba taarifa hiyo ilikuwa ya uongo huku akiashiria kuwa mwanahabari huyo alitumia fursa ya kuweza kupeperusha taarifa hiyo kumharibia jina meneja huyo.

Gavana Mbugua amewataka wakazi wa Nakuru kutokuwa na shaka kila wakati viongozi wanapotofautiana.

“Wakati kuna maoni tofauti kati ya gavana na kiongozi yoyote yule, wakazi wa Nakuru hawafai kuwa na wasiwasi mradi tu matamshi hayo hayalengi kuwagawanya watu wa Nakuru,” aliongeza Gavana Mbugua.