Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewaomba viongozi wote wa eneo la Kisii, ikiwemo Kaunti za Nyamira na Kisii kuacha tofauti zao za kisiasa na kujiunga pamoja kuletea wananchi maendeleo.
Wito huo umetolewa baada ya baadhi ya viongozi katika kaunti hizo mbili kufanya siasa kila mara huku wakiacha kufanya maendeleo jinsi walivyowahidi wapiga kura wakati walikuwa wakifanya kampeini.
Akizungumza siku ya Jumamosi mjini Nyamira, Gavana Nyagarama alisema wakati huu ni wa kufanya maendeleo kwa wananchi wala si wakati wa kufanya siasa.
Aliwaomba viongozi kuweka tofauti zao za kisiasa kando na kuzingatia maendeleo.
“Sisi viongozi tuliochaguliwa tuliwaahidi wananchi kuwa tutawafanyia maendeleo ambayo wanasubiri tuwafanyie hadi sasa,” alisema Gavana Nyagarama.
Aliongeza: “Mbona tusitimize ahadi tulizotoa na tuweke siasa kando? Siasa haziwezi sukuma eneo la Kisii mbele. Tunastahili tuje pamoja tujiunge tuache tofauti za kisiasa na tufanye maendeleo kwa wananchi wa eneo la Kisii, ili nasi tusonge mbele.”
Idadi kubwa ya wakazi wa eneo la Kisii wamekuwa wakiomba viongozi wao kuwafanyia maendeleo kila wakati jambo ambalo lilimlazimu gavana kuingilia kati na kujiunga nao kuomba viongozi kuleta maendeleo.