Wawakilishi wa wadi katika Kaunti ya Nyamira wamemtaka Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama kuunda kamati halisi ya kuchunguza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kaunti hiyo.
Hii ni baada ya kamati mbili katika bunge la kaunti hiyo kuundwa hapo awali ili kuchunguza maafisa sita waliosimamishwa kazi kufuatia madai ya ufisadi.
Kamati hizo ziliwasilisha ripoti tofauti ambazo haziambatini huku kila kamati ikiwa na uchunguzi wake.
Akizungumza katika makao ya bunge ya kaunti hiyo siku ya Jumanne, Spika wa bunge hilo, Joash Nyamoko, alisema kuwa ripoti amabazo ziliwasilishwa na kamati ya 'Selective committee' na ile ya 'Implementation committee' ambazo zilichaguliwa kuwachunguza maafisa hao waliosimamishwa kazi kwa madai ya ufisadi haziambatini jambo ambalo limeonekana kuwa kikwazo kwa uwazi kupatikana.
Nyamoko alimwomba Gavana Nyagarama kuunda kamati ya kuchunguza miradi yote inayotekelezwa katika kaunti hiyo.
Kulingana na Nyamoko, kamati ya 'Selective committee' ilitoa ripoti yake ya kuwaondolea maafisa wanne kati ya maafisa sita madai ya ufisadi huku ile ya 'Implementation' ikiwa na ripoti tofauti.
“Naomba gavana aunde kamati ya kuchunguza miradi yote ifanywayo na maafisa wa serikali katika kaunti hii,” alisema Nyamoko.
Ripoti hiyo ya 'Selective committee' ilikataliwa na bunge la Kaunti ya Nyamira huku wawakilishi wadi hao wakisema uchunguzi wake si halali.
Kwa upande wake, Gavana Nyagarama alisema kuwa ripoti ambayo ako nayo kwa sasa iko na mengi ya kuchunguzwa kabla ya kuiwasilisha na kuomba maafisa wake kuacha kufanya kazi ikiwa wameona itakuwa vigumu kwao kufanya kazi kikamilifu.