Gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amezindua feri mpya kwa jina la ‘Albert Nile’, ambayo inatarajiwa kusafirishwa na kutumika nchini Uganda.
Haya yalifichuka siku ya Jumatano kupitia akaunti ya Joho ya Facebook, ambapo alisema kuwa Feri hiyo ambayo ilitengenezwa jijini Mombasa na kampuni ya ‘Southern Engeneering’ itabomolewa na kusafirishwa hadi nchi ya Uganda, kisha iunganishwe tena kabla ya kuanza kazi.
"Feri hii itasafirishwa na malori 22 na kufikishwa nchini Uganda ambapo itatumika kusafirisha watu na bidhaa kwa ziwa la Albert," alielezea Joho kwenye akaunti yake.
Gavana huyo pia alichukua fursa hiyo kushukuru bodi na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwa kazi waliofanya, na kuahidi serikali yake itaendelea kusaidia wanabiashara kukuza biashara zao.
"Kaunti ya Mombasa itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa wanabiashara wa kaunti hiii katika kukuza na kuendeleza biashara zao. Pia nashukuru bodi na wafanyikazi wa kampuni ya ‘Southern Engeneering’ kwa juhudi zao walizowekeza kutengeneza feri hii," aliongezea Joho.
Pia aliitaja kazi hiyo kama njia mojawapo ya Mombasa kuwa imara kuleta maendeleo katika kanda hii ya Afrika Mashariki.