Wakazi wa eneo la Kabatini wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kuzindua mradi wa maji katika eneo hilo.
Mradi huo unatokana na kuchimbwa kwa visima viwili katika Shule ya upili ya Heroes na eneo la Kamugima ambayo ilifunguliwa rasmi na Gavana Mbugua.
Visima hivyo vitasambaza maji kwa zaidi ya wakazi elfu tatu wanaoishi katika eneo hilo.
Akizungumza siku ya Jumatano baada ya kufungua rasmi miradi hiyo, Mbugua aliwahakikishai wenyeji kuwa tatizo la maji halitashuhudiwa tena katika siku zijazo.
“Tunafurahia kuwa mradi huu utakuwa nguzo muhimu katika kusambaza maji katika eneo hili. Kutokana na mradi huu, swala la uhaba wa maji halitashuhudiwa tena na kila mmoja atapata fursa ya kutumia maji safi,” alisema Mbugua.
Mbugua pia aliahidi wakazi kuwa kaunti yake itaongeza mabomba ya maji ili wenyeji wapate maji kwa urahisi.
“Tutahakikisha kuwa mabomba ya maji yamewekwa katika makazi na shule mbalimbali katika eneo hili,” aliongezea Mbugua.
Gavana huyo pia aliwahakikishia wananchi usalama wao huku akisema kuwa serikali yake imetenga fedha za kununua taa za mitaani za sola.
“Shughuli ya kuwekeza taa za sola zitaendelea kote katika kaunti hii ili usalama uimarishe kwa saa 24,” alisema Mbugua.