Wanyakuzi wa ardhi wanaoendelea kunyakuwa ardhi za umma kwenye kaunti ya Nyamira wameonywa vikali na gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama.
Akiongoza hafla ya kusherehekea siku ya Mashujaa nchini kwenye uwanja wa michezo wa Nyamaiya, Gavana Nyagarama aliwaonya vikali wanyakuzi hao huku akisema kwamba serikali yake kwa ushirikiano na ile ya kitaifa hazitosita kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wenye hulka hizo.
"Nawaonya vikali watu wenye hulka za kunyakua ardhi za umma ambazo hutengewa miradi mbalimbali, na ninasisitiza kwamba serikali yangu na ile ya kitaifa hazitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria," alisema Nyagarama.
Gavana huyo aliongeza kusema kuwa serikali yake ilitenga kima cha shillingi millioni 25 kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka wa 2015-2016, pesa zitakazotumika kujenga uga wa michezo wa Nyamaiya ili uwe ukitumiwa kwa maonyesho ya kilimo kwenye kaunti hiyo.
"Serikali yangu ilitenga shillingi millioni 25 kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka wa 2015-2016, pesa zitakazotumika kujenga uga wa michezo wa Nyamaiya," aliongeza Nyagarama.
Gavana Nyagarama aidha alisema kwamba serikali yake ina mipango ya kujenga maktaba ya umma itakayowasaidia wanafunzi kwenye masomo yao, na kudai kwamba tayari afisi yake ishawasiliana na afisi ya huduma za maktaba ya kitaifa na kuna uwezekano wa maktaba hiyo kuanzishwa hivi karibuni.
"Serikali yangu ina mipango ya kujenga maktaba ya umma humu nyamira ili kuwasaidia wananchi hasa wanafunzi kwenye masomo yao, na tayari tushawasiliana na afisi ya huduma za maktaba nchini na jinsi mambo yalivyo, huenda tukawa na maktaba hiyo hivi karibuni," alihoji Nyagarama.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wananchi wa matabaka mbalimbali, mawaziri, makatibu, spika wa bunge hilo na wawakilishi wa wadi.