Wakazi wa kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya Gavana wa kaunti hiyo James Ongwae kuahidi kuimarisha sekta ya afya.
Gavana huyo alisema kuwa hospitali zote za level four zitawekwa mashine mbambali ili wananchi waweze kuhudumiwa kwa urahisi kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika uwanja wa michezo wa Nyamache ulioko eneo bunge la Bobasi, Gavana Ongwae alisema hospitali zote za kiwango cha level four zitawekwa mashine mbalimbali za kupima magonjwa ya kila aina pamoja na dawa za kutosha ili kuimarisha sekta ya afya.
Wakati huo huo, Gavana Ongwae alisema zahanati zote zilizojengwa kupitia fedha za hazina ya ustawi ya maeneo bunge hapo mbeleni kabla ya serikali za ugatuzi kuingia mamlakani zitafunguliwa hivi karibuni ili wakazi wa kaunti hiyo waweze kunufaika na huduma ya matibu karibu na kwao.
“Serikali yangu imeweka mikakati kabambe ya kufungua zahanati zote na kuweka dawa za kutosha ili wananchi wawe wakipata matibabu karibu na wanapoishi,” alisema Ongwae.
Aliongeza: “Hamutakua munalazimika kuenda kutafuta huduma ya matibabu katika hospitali ya rufaa ya Kisii maana mtakuwa mkitibiwa karibu na mnapoishi."
Gavana Ongwae aliandamana na waziri wa afya kaunti ya Kisii Sarah Omache na maafisa wengine katika serikali ya kaunti hiyo pamoja na wawakilishi wa wadi mbalimbali.