Gavana wa kaunti ya kisii James Ongwae amesema serikali ya kaunti hiyo itajenga mkahawa mkubwa wa kisasa katika eneo la Tabaka iliyoko eneo bunge la Mugirango Kusini ili watalii wawe wanakula na kupumzikia katika mkahawa huo.
Hii ni baada ya watalii wengi kuendelea kuzuru eneo hilo la Tabaka ambapo uchongaji wa vinyago hufanywa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo.
Akiongea siku ya Jumanne katika mji wa Kisii, Ongwae alisema kuwa mkahawa huo utajengwa hivi karibuni katika eneo la Tabaka.
Alisema kuwa tayari mikakati imeanzishwa kuhusiana na ujenzi huo kama njia mojawapo ya kukuza uchumi wa kaunti ya Kisii.
Eneo la Tabaka hujulikana kama sehemu ya watalii ambao huzuru eneo hilo kujionea jinsi vinyago huchongwa jambo ambalo limepelekea kaunti ya kisii kujulikana nchini kupitia vinyago hivyo.
“Serikali yangu itajenga mkahawa katika eneo la Tabaka maana tumegundua kwamba wale wageni na watalii ambao huzuru eneo hili hawana pa kupumzika. Ujenzi huo utaanza hivi karibuni,” alisema Gavana Ongwae.
Aidha, Gavana Ongwae aliongezea kuwa kiwanda cha miwa kitajengwa katika eneo bunge la Mugirango Kusini ili wakulima wa miwa waweze kufanya biashara yao kwa urahisi.