Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alifungua rasmi mradi wa maji ya kisima katika Wadi ya Tabaka ilioko eneo bunge la Mugirango Kusini.
Mradi huo ulifunguliwa siku ya Jumanne katika wadi ya Tabaka baada ya kisima hicho kilochochimbwa kutumia pesa za kaunti ya Kisii katika Shule ya Msingi ya Tabaka kukamilika.
Maji hayo yatawasaidia wakazi wa wadi hiyo ya Tabaka pamoja na shule zote za wadi hiyo. Ukosefu wa maji yamekuwa kero kubwa kwa wakazi wa wadi hiyo kwa muda sasa, jambo ambalo limepata suluhu kupitia serikali ya Kaunti ya Kisii.
“Serikali yangu ilisikia kilio chenu maana mlikuwa mkilia kila wakati kwamba hamna maji ndio maana leo hii nimeanzisha rasmi matumizi ya maji haya ili muyatumie katika wadi hii,” alisema Gavana Ongwae.
Wakazi wa wadi hiyo walionekana wakiwa na furaha kwa gavana Ongwae huku wengine wao wakimwomba gavana huyo kuweka mabomba ambayo yatapitisha maji mpaka shule za eneo hilo na baadhi ya miji kwani wadi hiyo ya Tabaka ni kubwa ambayo itawapelekea kutembea mbali kuchota maji hayo ambayo yaliwekwa katika Shule ya Msingi ya Tabaka
“Namwomba gavana atuwekee mabomba ili kila sehemu ipate maji maana kama mimi natoka huko chini eneo la Nyachenge na mlima ulioko kufika hapa kwa shule ya Tabaka kuchota maji itakuwa mbali na kibarua kigumu kwangu,” alisema Beatrice Kerama, mkaazi.
Matamshi ya mkazi huyo yaliungwa mkono na wakazi wengi wa wadi hiyo, jambo ambalo gavana aliitikia kufanya kabla ya mwaka huu kukamilika.
Kwengineko, shughuli ya kuwapima ugonjwa wa ukimwi kwa wakaazi wa eneo hilo ilifanyika katika uwanja huo wa Shule ya Msingi ya Tabaka kupitia mradi ya Beyond Zero campaign.