Wafanyibiashara wa eneo la Keumbu eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya gavana wa kaunti hiyo James Ongwae kutenga mahala na kuwajengea soko mpya ili wafanyibiashara hao waweze kuendelea na biashara.
Haya yanajiri baada ya visa vingi vya ajali kuendelea kushuhudiwa katika eneo hilo kwani wafanyibiashara hao wamekuwa wakifanyia biashara zao kando kando mwa barabara ya kutoka Kericho kuelekea Kisii ambayo hupita katika eneo la keumbu.
Akiongea siku ya Alhamisi katika eneo la Keumbu gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae alisema serikali yake imefanya ujenzi wa soko mpya ili wanabiashara wapate mahala pa kufanyia biashara yao.
Gavana Ongwae aliandamana na maafisa wakuu wa serikali kukagua ujenzi wa soko hilo ambalo liko karibu kukamilika.
Wakati huo huo, Ongwae aliahidi wakaazi wa eneo la Keumbu kuwa serikali ya Kisii italipa deni ya shillingi milioni nne ili wakaazi wa eneo hilo warudishiwe maji yaliyokatwa hapo mbeleni kufuatia deni hilo.
Gavana Ongwae pia alitoa trakta moja itakayotumika kuondoa uchafu katika soko hilo.
“Nataka wakaazi wa kaunti ya Kisii wafurahie serikali za ugatuzi. Nawaahidi nitaendelea kuwafanyia maendeleo ili kila mtu aridhike. Nitahakikisha nimefanya kazi muliyonichagua kufanya kikamilifu,” alisema Ongwae.