Kama njia mojawapo ya kuitangaza kaunti ya Kisii katika masuala ya uwekezaji, mmoja wa waandishi habari wakongwe Andrea Morara amezindua gazeti la kila mwezi katika mji wa Kisii.
Akizungumza siku ya Jumatatu, Morara, ambaye amewahi kuwa mhariri wa gazeti la Nation na baadaye kuenda ng’ambo, alisema kuwa gazeti hilo ambalo litafahamika kama The Gusii Chronicle litakuwa la kila mwezi na litakuwa linaangazia kaunti za Nyamira, Kisii, pamoja na kaunti nyingine kutoka maeneo ya Nyanza Kusini kama Migori na Siaya.
Morara ambaye pia ni mkurugenzi na mwahariri mkuu wa gazeti hilo aliwataka viongozi wa kaunti ya Kisii kushirikiana na kuinua uchumi wa wakaazi hasa vijana ambao alitaja kuwa na idadi kubwa mno; takribani asilimia 70 kwa kuwapa kazi na wengine kutafutiwa njia ya kujikimu kama mikopo ya kufanyabiashara.
“Vijana ndio nguzo ya kaunti hii ya Kisii na Nyamira na sharti tuwashike mikono ili kwa kutumia vyombo na taasisi za habari kama hii, hakuna mtu anakuja kuboresha kaunti zetu, inaanza na sisi mwanzo,” Bwana Morara alisema.
Kwingineko meneja mhahariri wa gazeti hilo Jimmy Achira, aliwapa waandishi wa habari kutoka eneo kuu la Nyanza kuanza kufanya utafiti wa kutosha na kuandika habari za kuridhisha na za maendeleo kutoka kaunti zote ambazo gazeti hilo litakuwa linaangazia.
Pia aliwaomba wafanyabiashara wote kutoka mji wa Kisii na Nyamira kuweka ushirikiano mwafaka kati yao na vyombo vya habari ili kuendelea kuvipandisha viwango vya elimu ili kupitia elimu, jamii itakuwa kiuchumi.