Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Mombasa wameihimiza serikali kuheshimu agizo la mahakama na kuwalipa walimu nyongeza yao ya mishahara wanayodai.
Wakiongozwa na Seneta wa kaunti ya Mombasa Hassan Omar, Viongozi hao wamesema kwamba serikali inafaa kuchukua jukumu la kuwapa walimu kwani ni haki yao kikatiba, huku akisema kwamba wizara ya hazina ya fedha nchini iko na pesa za kuwalipa walimu.
Akiongea mjini Mombasa baada ya swala maalum ya Eid siku ya Alhamsi, Omar alisema kwamba iwapo serikali imeshindwa kuliongoza taifa hili, basi wabanduke mamlakani na kupisha viongozi wenye uwezo wa kumudu gharama za wananchi sambamba na kuwatendea walimu haki yao pamoja na wanafunzi.
“Sioni kwa nini serikali idinde kutoa fedha na kuwalipa walimu nyongeza yao na wizara ya fedha iko na pesa za kutosha. Cha msingi ni walimu walipwe na wanafunzi wapate masomo kwani ni haki yao kikatiba kupata msingi bora wa elimu,” alisema Omar.
Aidha amepinga madai ya kuwa kampeni iliyozinduliwa na mrengo wa Cord kuishiniza serikali kuwalipa walimu nyongeza yao kuwa haitasadia, akisema kwamba viongozi wa mrengo wa Cord watahakikisha kuwa serikali imeliwajibikia swala hilo.
“Mrengo wa Cord haujazindua kitu na ukashindwa. Tumeandaa mikakati mwafaka ya kufanikisha kampeni tuliyozindua jana (Jumatano) ya kuihimiza serikali kuwajika vyema katika kuwatekelezea wananchi maendeleo pamoja na kuwalipa walimu mishahara yao. Hatutakwamia hapo, tutazidi kuhakikisha kwamba taifa hili limesonga mbele kimaendeleo na kidemokrasia,” aliongeza.
Siku ya Jumatano, mrengo wa Cord ulizindua rasmi kampeni yao ya kuishinikiza serikali kuwajibikia vyema majukumu yao ya kuliongoza taifa hili pamoja na kuwalipa walimu mishahara yao wanayodai kabla ya kusambaratisha shughuli za masomo nchini.