Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kaunti ya Mombasa kwa ushirikiano na Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani inalenga kuwafikia zaidi ya akina mama hamsini kila mwaka ili kujaribu kupunguza idadi ya wanawake ambao wameathirika na shida ya fistula.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika hafla ya kuanzisha rasmi kitengo cha matibabu hayo kwa wanawake ambao wana shida hiyo ya fistula kwenye hospitali hiyo, mkurugenzi mkuu wa matibabu kwenye hospital hiyo ya rufaa, Dkt Khadija Shikeli, alisema kuwa wanawake wengi ambao wameathirika hawajitokezi kwa kuogopa kuchekwa na jamii na wale ambao wanako karibu nao.

Aliwashauri waathiriwa kutoogopa na kukumbuka kuwa maradhi hayana mwenyewe kwa sababu yanampata kila mwanadamu.

Aliwahimiza waende katika hospitali za mikoa au wilaya kupewa tiba kwa kufanyiwa upasuaji na kupewa dawa za kuwaponya.

Daktari huyo alisema kuwa nia yao ni kuona kuwa shida hiyo ambayo imewaletea kina mama wengi shida na hata wengine kufukuzwa kutoka ndoa zao inaangamizwa kabisa.

“Tuna nia ya kuhakikisha kuwa kina mama wanakaa na ustarabu na stara ambayo inawafaa badala ya kuugulia katika maboma yao wakiteseka na shida hiyo ambayo ina tiba,” alsiema Shikeli.

Aidha, alisema kuwa wana azma ya kuandaa shughili hiyo kila mwaka kwa ushirikiano na kaunti ya Mombasa na mashirika mengine ya kimataifa.

Shughuli hiyo iliweza kupokea zaidi ya kina mama ishirini na watano na ilifanywa kwa ushirikiano na mashirika yasiyokuwa ya serikali kutoka ng’ambo na mashirika mengine kutoka mjini Mombasa ikiwemo shirika la kimataifa la Amref.