OCPD wa Nakuru bwana Bernard Kioko amesema visa vya uhalifu mjini Nakuru vimepungua kwa kiwango kikubwa mno kutokana na mahubiri ya mara kwa mara yanayoandaliwa mjini humo.
Akizungumza katika ofisi yake siku ya Jumatano, OCPD Kioko ambaye pia ni mhubiri alisema kwamba mahubiri hayo ambayo hufanyika kati ya saa saba na saa nane mchana kila siku ya wiki yameimarisaha sheria za kijamii kwa kiwango kikubwa.
Hii imetokana na uimarishaji wa utangamano kati ya maafisa wa polisi na umma. Kwa muda mrefu uhusiano kati ya maafisa wa polisi na wananchi haujakuwa murua hivyo basi uhasama huo huchangia kwa njia moja ama nyingine katika kupunguza uenezaji wa uhalifu.
“Tuna uhusiano murua kati yetu na wananchi wa eneo hili kwa sababu mimi huwahubiria kila siku ya wiki jambo ambalo limeweza kupunguza uhasama uliokuwepo baina ya wannanchi na maafisa wa polisi hapo mbeleni,” alisema afisa Kioko.
Bwana Kioko aliongezea kwamba kanisa lake limefunguliwa kwa kila mtu ambaye angependa kujiunga naye wakiwemo maafisa wa polisi kutoka vituo vingine.
“Tangu nije Nakuru na kuanza kuhubiri, visa vya uhalifu vimedidimia mno. Jambo hili linaashiria umuhimu wa neno la Mungu katika masiha ya kila mtu,” alisema Kioko.
Kioko amabaye alianza kuhubiri mwaka wa 1996 amekuwa akihubiri katika maeneo yote ambayo ametumwa kuhudumu kama polisi.
Hata hivyo, Kioko alikiri kwamba amekumbwa na changamoto nyingi zikiwemo kudhalilishwa na maafisa wengine haswa alipoanza kazi ya kuhubiria watu, lakini anafuraha kwani walianza kumuunga mkono baada ya kugundua kwanba juhudi zake zilikuwa zikizaa matunda mema.