Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa wa masuala ya mazingira katika Kaunti ya Kisii ameshtumu afisa aliyeidhinisha shughuli ya kuchimbua na kuchonga mawe katika sehemu ya Nyambera viungani mwa mji wa Kisii. 

Afisa huyo, Samson Pokea amewataka vijana wanaofanya shughuli hiyo kumakinika zaidi kwani mawe na udongo wa eneo hilo uko mwepesi mno kwa sababu ya kuchimbuliwa kila mara.

Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano alipokuja kutathmini hali ya timbo hilo baada ya mtu mmoja kuangukiwa na jiwe kubwa na kuaga dunia, Pokea alisema kuwa watajadili suala hilo na kutoa uamuzi ambapo huenda wakafunga timbo hilo la kuchonga mawe na shughuli zote kusitishwa kuendelea mahali hapo.

"Afisa aliyehusika kwenye mradi huu alikuwa hajafuzu na huenda tutafunga shughuli na timbo hili baada ya kujadiliana kama afisi husika," alisema Pokea.

Kulingana na baadhi ya watu wanao chonga mawe katika timbo hilo, marehemu alikuwa akiendelea kuchimba mawe kwenye shimo moja alipofunikwa na mawe yaliyoporomoka kutoka juu na kumuua papo hapo.

Ilichukua trakta ya serikali ya kaunti ya Kisii zaidi ya saa moja kutoa mwili wa marehemu uliochukuliwa katika hifadhi ya wafu ya hospitali ya Kisii level six.

Wakazi wa sehemu hiyo kwa upande wao waliitaka serikali kuwatafutia vijana njia mbadala ya kujikimu kimaisha ili wawache kazi hatari kama hiyo.