Share news tips with us here at Hivisasa

Takriban vitambulisho 43,381 vimerundikana katika afisi za usajili wa watu katika eneo la North-Rift vikisubiri wenyewe kuvichukua.

Mshrikishi wa usajili wa watu katika eneo hilo Samuel Sagala amesema baadhi ya vitambulisho hivyo vimekaa katika afisi hizo kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Sagala alisema idadi kubwa ya vitambulisho hivyo viko katika afisi za usajili wa watu katika kaunti ya Uasin Gishu.

Miongoni mwa kaunti nyingine ni Turkana, Pokot Magharibi na Transzoia.

Akizungumza afisini mwake mjini Eldoret, Sagala alisema vitambulisho 24,757 vimekuwa afisini humo kwa takriban mwaka mmoja, ambapo vitambuisho 10,929 kati ya vitambulisho hivyo ni vya wale watu ambao walituma maombi ya kuvipokea kwa mara ya kwanza.

Vitambulisho vingine 13,808 ni vya wale watu ambao walivipoteza vitambulisho vyao na kutuma maombi ya kuvipokea tena.

“Sehemu kubwa ya vitambulisho hivi ni vya wale vijana chipukizi ambao wametuma maombi ya kuvipokea kwa mara ya kwanza. Tunaomba wahusika watembelee afisi zetu katika kaunti zao ili wachukue vitambulisho vyao,” alisema Sagala.

Pia alisema kutokana na hatua ya idara hiyo kukumbatia teknolojia ya kisasa, mchakato wa kutoa vitambulisho huendelezwa kwa haraka baada ya kutuma maombi, kinyume na hapo awali ambapo ilikuwa inachukua muda mrefu kabla ya kuwa tayari.

“Kwa mwezi huwa tunatoa takriban ya vitambulisho 6,000, na kuna haja ya wadau kushirikiana zaidi ili kuboresha utoaji vitambulisho katika maeneo kama Turkana, West Pokot na Transzoia,” alisema.

Kiongozi huyo alisifia kaunti ndogo ya Pokot kaskazini kwa kujizatiti na kutoa vitambulisho 8,000 kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja.