Huenda vijana ambao wanajihusisha kwenye operesheni ya kuwahangaisha wakazi kwenye Kaunti ya Kisii kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na kifungu cha usalama kwa jamii.
Kwenye hafla ya kukusanya maoni kutoka kwenye umma na maafisa wa polisi ulioandaliwa siku ya Jumatano wiki iliyopita, katika ukumbi wa Gusii Cultural, na kusimamiwa na tume ya kuchunguza na kusimamia usalama na vitendo vya maafisa wa polisi IPOA, wengi waliochangia waliyalaumu makundi hayo mojayapo likiwa lile la Sungusungu ambalo lilishtumiwa mno na umma kwa kuhudumu kama polisi katika kaunti hiyo.
Akiongea kwenye warsha hiyo, mjumbe wa bodi katika shirika hilo la IPOA Tom Kagwe, alisema kuwa sheria za kusimamia ulinzi wa jamii 'Community Policing' zililaumiwa kwa kutokuwa na makali ya kuwashtaki vijana hao ambao wanahangaisha jamii.
"Sheria itaanza kutekelezwa ili kuyatokomeza makundi haramu ambayo yamekuwa yakiwatishia wakazi usalama wao, kwa sababu tumeambiwa wengine hata wanashirikiana na maafisa wa polisi ambayo ni kinyume na sheria," alisema Kagwe.
Kwa upande wake, afisa wa kitengo cha sheria cha IPOA, James Olola, alisema kuwa sheria ya kutetea haki za umma itaanza kufanya kazi hivi karibuni na kusema kuwa wale wanaojuhusisha na makundi hayo kama SunguSungu watakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria.
Kundi la Sungusungu limeshtumiwa katika kaunti ya Nyamira pamoja na ile ya Kisii kwa kuhudumu kinyume na sheria na kusemekana kuwa wengi wa vijana kwenye kundi hilo wamekuwa wakiwapiga watu na hata kuhusika katika mauaji ya baadhi wakazi.