Mshukiwa mmoja wa kundi la kigaidi la Al Shabab anayetuhumiwa kuwa miongoni mwa waliotekeleza shambulizi la chuo kikuu cha Garissa amenyimwa dhamana ya milioni kumi aliyopewa awali na mahakama kuu chini.
Mahakama hiyo ilifutilia mbali dhamana hiyo siku ya Alhamisi Julai 30, ambayo iliitoa tarehe 14 mwezi huu baada ya kubainika kuwa mashahidi watano wa kesi hiyo walikuwa wamepoteza maisha yao katika shambulizi la kigaidi la Lamu siku moja baada ya dhamana hiyo kutolewa.
Jaji wa mahakama hiyo Martin Muya ndiye aliyekuwa amempa Mohamed Khalid dhamana hiyo tarehe 14 mwezi huu na alisema ameamua kuifutilia mbali kwa kuzingatia ombi la kiongozi wa mashtaka kuhusu kesi hiyo.
Jaji Muya alisema sababu za usalama wa mashahidi zilizotolewa na upande wa mashtaka ndizo zilizomfanya kufanya uamuzi huo wa kutomwachilia mshukiwa kwa dhamana kwani huenda angetatiza ushahidi wa kesi hiyo.
“Nimechukulia kwa uzito maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka na nimechukulia swala hili kwa uzito mkubwa, na hivyo nimeamua kufutilia mbali dhamana hiyo,” alisema jaji.
Shambulizi hilo la Garissa liliwaua watu wasiopungua 147 katika chuo cha Garissa, na kilisababisha chuo hicho kufungwa kwa muda na wizara ya elimu huku wanafunzi wa chuo hicho wakijiunga na chuo kukuu cha Moi mjini Eldoret.