Mmoja wa majambazi waliotoroka kutoka kwa Gereza kuu la Naivasha mapema mwaka huu amekamatwa mjini Gilgil siku ya Ijumaa.
Akithibitisha kisa hicho, afisa wa utawala anayesimamia uhalifu Inspekta John Waweru aliyeongoza oparesheni hiyo kupitia kwa njia ya simu, alisema mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la Bondeni kufuatia vidokezo kutoka kwa umma.
Waweru alibaini kwamba baada ya kugundua uwepo wa maafisa wa polisi, mshukiwa huyo ambaye jina lake halisi bado halijabainishwa alijaribu kutoroka lakini maafisa wa polisi walifanikiwa kumkamata.
Aliongeza kwamba mshukiwa huyo amekuwa akijitambulisha kwa majina mawili tofauti kama David Mwangi almaarufu Kajunior au kwa majina ya John Mbugua.
Kulingana na Waweru, mshukiwa huyo alikuwa amehukumiwa pamoja na jamaa wengine wawili baada ya kupatikana na hatia ya kuiba bastola ya Naibu OCPD wa Gilgil lakini alifanikiwa kutoroka kutoka kwa gereza kuu la Naivasha mapema mwaka huu.
Waweru aidha alisema tangu wakati huo, maafisa walianza msako wa kumtafuta jamaa huyo, huku akitaja kukamatwa huko kwa mhalifu huyo kama tukio kuu la kukabiliana na uhalifu katika eneo hilo.
Kwa sasa, mshukiwa huyo anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Gilgil akisubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.