Jamii ya watu wanaoishi na ulemavu katika eneo la Pwani wamelishinikiza shirika la huduma za feri nchini kutenga mahali maalum pa kuabiri feri kwa jamii hiyo.
Kulingana na mshirikishi mkuu wa jamii hiyo eneo la Pwani Hamisa Zaja, hatua hiyo itasadia pakubwa jamii hiyo ya walemavu kuepukana na misongomano wakati wa kuabiri feri kutokana na hali yao ya kimaumbele.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatau, Zaja amesema kwamba jamii hiyo hukumbwa na changamoto nyingi katika kivuko cha feri cha Likoni wakati wa kuabiri feri, na akasema kwamba hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa ili kuzuia mikasa kutokea katika kivuko hicho.
“Walemavu hupitia changamoto nyingi sana wakati wakiabiri feri kuvuka katika kivuko cha feri cha Likoni. Watu husukumwa na kuumizwa kutokana na hali ngumu ya walemuvu kushindwa kumudu msukumano huo. Hili ni jambo la kusikitisha na linafaa kuangaziwa kwa haraka,” alisema Zaja.
Aidha, amewataka wasimamizi wa shirika hilo la huduma za feri nchini kutafuta mbinu mbadala za kuisaidia jamii hiyo ya walemavu ili kuepukana na misongamano mikubwa pamoja na kujeruhiwa wakati wakazi wanaposukumana wakiabiri feri katika kivuko hicho cha feri cha Likoni mjini Mombasa.
“Tungewaomba viongozi na wasimamizi wa shirika la huduma za feri nchini watengee walemavu mahali maalum pa kuabiri feri ili kupukana na mikasa kutokana na misongamano inayoshughudiwa wakati watu wakiabiri feri,” aliongeza Zaja.
Mapendekezo ya mshirikishi huyo mkuu yamejiri baada ya watu kujeruhiwa wakati wakazi wakisongamana katika kivuko hicho cha feri wakiabiri feri, hatua ambayo imepelekea wasimamizi wa shirika hilo kupendeleza kununulia feri zengine mpya.