Huku mashirika pamoja na serikali za kitaifa na zile za kaunti zikipiga vita dhidi ya maradhi hatari ya Ukimwi, jamii imehimizwa kushikana mikono kwa kutokomeza janga hilo kwa kuenda kupimwa katika vituo vya hiari kwenye hospitali na maeneo mengine ya mashirika yasiyo ya serikali.
Akiongea siku ya Ijumaa kwenye mahojiano na waandishi wa habari, msimamizi mkuu katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini, Dkt Thomas Oirere, alisema kuwa watu sharti wachukue jukumu la kuenda katika vituo ili kupimwa na kujua hali yao kama njia mojawapo ya kuona kuwa maambukizi yanapungua.
Dkt Oirere aliwataka vile vile wale ambao tayari wamepatikana na maradhi hayo, kuendelea kutumia dawa za kupunguza makali ili kurefusha maisha yao.
Aidha, aliongezea kuwa Kaunti ya Kisii ipo katika nambari ya tano kwenye orodha ya miongoni mwa zile kaunti ambazo zina viwango vya juu vya maambukizi hayo.
“Sharti jamii yote ije pamoja nakuacha kuwabagua wale ambao tayari wamepatikana na maradhi hayo, kwa vile huwa inawafanya wengine kuhisi kuwa hawana umuhimu katika dunia na hata kusababisha wengine kufa kabla ya wakati wao kuwadia,” alisema Dkt Oirere.
Kwa upande wake, afisa mmoja ambaye aliwakilisha shirika lisilo la kiserikali la Wezesha OVC, Bwana Isaiah Onyango alisema kuwa sharti waathiriwa waweze kutumia dawa zao mara kwa mara kulingana na maagizo ya daktari.
Aliiomba jamii kushiriki katika kuwapa upendo wale tayari wamepatikana na maradhi hayo na kukoma kuwabagua.