Jamii ya Abagusii imetakiwa kuacha mila zilizopitwa na wakati na kukumbatia maisha ya kisasa na wakazi wote kushikana katika vita dhidi ya ukeketaji wa watoto wa kike.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua rasmi bodi simamizi ya ushauri itakayojihusisha na vita dhidi ya dhuluma kwa watoto siku ya Jumanne, mkurugenzi wa shirika la kupigana na ukeketaji wa watoto wa kike, ADRA Kenya, Mary Kwamboka alisema kuwa wengi wa wazazi wamekuwa na mtindo wa kutetea mila kila kunapozuka pingamizi kuhusiana na kuketwa na watoto.
Aliwata akina mama kushirikiana na kina baba na jamii kwa jumla ili kupigana na maovu kama hayo ambayo hufanyika kila mara.
Kwamboka alisema kuwa wengi ambao hujihusisha na ukeketaji hufanya zoezi hilo kwa siri, na hushirikiana na baadhi ya wasimamizi wa Jamii, hali ambayo huwa vigumu kwao kufuatilizia masuala hayo.
Hata hivyo, alisema kuwa kupitia ushirikiano na mashirika mengine yasiyokuwa ya serikali na yale ya kijamii, angalau wameweza kupunguza visa hivyo na kuwashukuru wazazi ambao wameonyesha azimio la kung’oa zongobwingo hilo kutoka miongoni mwa jamii ya wakisii.
Afisa huyo aliipongeza serikali ya kaunti ya Kisii kwa kuwapa msaada shida inapotokea kwa kuwapa taarifa muhimu ya kuwasaidia watoto wa kike ambao wanajipata katika zogo hilo la kuketwa bila ihiari yao.