Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu kamishena wilayani Kenyenya eneo bunge la Bomachoge Borabu, Chaunga Mwachaunga, amesema maafisa wa polisi watatumia nguvu ikiwa wakazi wanaopakana na jamii ya Maasai wa Kaunti ya Narok hawatakomesha vita baina yao.

Wito huo umetolewa kufuatia fujo na uharibifu wa mali kuendelea kwa muda mrefu sasa kati ya kabila hizo mbili.

Jamii ya Kisii inadai kuwa jamii ya Maasai huiba ng’ombe wao na kuchoma miwa yao jambo ambalo limepelekea fujo na vita kuendelea kwa muda mrefu.

Jamii hizo mbili zimepewa mkataa wa kukomeza vita hivyo kwa majuma mawili yajayo, ama polisi watumie nguvu.

Akizungumza siku ya Jumamosi katika hafla iliyoandaliwa ili kuwaleta pamoja jamii hizo mbili, Mwachaunga aliomba Jamii hizo kukomesha vita kwa wiki mbili zijazo au wachukuliwe hatua kali za kisheria na polisi kutumia nguvu.

“Wiki mbili zikikamilika kabla hamjakomesha vita, mtakiona kile nimesema leo. Polisi watatumia nguvu na sheria kali zitachukuliwa dhidi yenu,” alisema Mwachaunga.

Victor Osoro, kutoka Jamii ya Kisii, aliomba wakisii watatu waliotiwa mbaroni hapo mbeleni kufuatia vita hivyo waachiliwe huru ili waweze kurudi nyumbani.