Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Ali Joho ameahidi kushirikiana na maafisa wa usalama katika kukabiliana na ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya ili kuwanusuru vijana wadogo wanaodaiwa kuathirika na janga hilo.

Akiwahutubia wakazi wa Kaunti ya Mombasa siku ya Jumanne, Joho alisema kuwa takwimu zimeonyesha kuwa asilimia kubwa ya vijana katika kaunti hiyo ya Mombasa wameathirika na utumizi wa dawa za kulevya na lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika wakuu ili kusitisha ulanguzi huo.

“Hatua ya kuwakamata watumizi na walanguzi wadogo wa dawa za kulevya kamwe hazitasaidia kupunguza kuenea kwa mihadarati. Lazima walanguzi wakuu kutiwa mbaroni ili kuwanasuru vijana wadogo waliyojitosa katika janga hilo,” alisema Joho.

Joho amesema kwamba serikali yake itahakikisha kuwa utumizi wa dawa za kulevya katika kaunti hiyo unasitishwa kwa asilimia kubwa na vijana waliojitosa katika utumizi wa dawa hizo wanapelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia ili vijana hao waweza kuzisaidia jamii zao.

“Wale wote walijoitosa katika utumizi wa dawa za kulevya lazima washikwe na wapelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia ili nao waweze kuwasaidia wazazi wao na ndugu zao kule mashinani. Serikali ya kaunti iko tayari kuwasaidia vijana hao kutoka katika masaibu hayo,” alisema Joho.

Joho aliunga mkono hatua ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuviangamiza vyombo vyote vya usafiri vinavyotumika kusafirisha dawa za kulevya humu nchini na kusema kwamba hatua hiyo itasitisha kuenea kwa mihadarati humu nchini na hususan katika Kaunti ya Mombasa.

Kufikia sasa zaidi ya vijana 60 wametiwa nguvuni na maafisa wa usalama katika oparesheni kali ya kusaka dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwashinikiza viongozi wa kisiasa kushirikiana na maafisa wa usalama katika kuwakabili walanguzi wakuu.