Viongozi wa Mombasa wamesisitiza ni lazima hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa, TUM walioharibu mali ya umma.
Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari siku ya Jumtatu, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisema mipango imewekwa kuhakikisha mali hiyo inafidiwa ima kupitia kwa wanafunzi ama kwa taasisi yenyewe.
Joho aliagiza orodha ya wanafunzi waliotekeleza uhalifu huo ili waweze kununua magari mawili waliyoyachoma.
Aidha, mbunge wa Mvita, ambapo taasisi hiyo iko, Abdulswamad Nassir alisema wataweka kanuni kwamba mwanafunzi yeyote atakayetaka msaada wa karo ama msaada wowote wa kielimu lazima awe na barua ya chuo chake kuonyesha ni mwanafunzi mwenye nidhamu.
Abdulswamad ameeleza kwamba licha ya kwamba watayashughulikia matatizo ya wanafunzi hao, kaunti kwa sasa inafaa kuwachukulia hatua waliotekeleza uhalifu huo.
Mapema siku ya Jumatatu, wanafunzi hao waliteketeza malori mawili ya takataka yanayoegeshwa pembezoni mwa barabara.