Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa anayesimamia mipango katika Shirika la 'Centre for Enhancing Democracy and Good Governance' (CEDGG) amesikitishwa na matukio ya wizi wa mtihani wa kitaifa wa KCSE unaoendelea kwa sasa.

Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye mahojiano na mwandishi huyu mjini Nakuru, Masese Kemunche alilaumu serikali ya kitaifa kupitia Wizara ya elimu kwa kutoshughulikia swala hilo kikamilifu na kwa kutolipa uzito unaostahili.

“Tunasikitika kwamba serikali haichukulii swala hili kama la muhimu. Mitihani haiwezi kuibiwa bila ya ushirikiano au bila ya wasimaizi wa mitihani hiyo kuhusika. Ni lazima tatizo litafutwe liko wapi kuanzia kwa baraza la kitaifa la mitihani na wote wanaohusika katika mtihani huo wa kitaifa,” alisema Kemunche.

Kulingana na Kemunche Waziri wa elimu Profesa Jacob Kaimenyi ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama waziri.

“Anaposema mtihani haujaibiwa na mitaindao ya kijamii imejaa makaratasi ya mitihani iliyoibiwa, anajaribu kueleza wakenya nini? Waziri huyu ameletea nchi hii aibu kubwa,” alisema Kemunche.

Aidha, afisa huyo alikubaliana na usemi wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB kuwa waziri Kaimenyi anafaa kulaumiwa kutokana na wizi huo wa mtihani wa KCSE na kuwajibikia swala hilo mara moja.