Mkurugenzi wa watoto wa chekechea kaunti ya Nyamira Rechael Okong’o amesema kamati imechaguliwa ili kuangalia jinsi viwango vya elimu vitainuliwa haswa kwa masomo ya watoto wachanga.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, mkurugenzi huyo alisema kama njia mojawapo ya kuinua viwango vya masomo kwa watoto hao wa chekechea, waliona ni vizuri kamati ichaguliwe ambayo itakuwa ikishughulikia viwango hivyo vya elimu kwa kuzunguka kila shule iliyo na watoto wa chekechea ili kukabidhi serikali changamoto watoto hao hupitia ili kushughulikiwa.
“Hii kamati ilichaguliwa ili iwe inashughulikia masomo ya watoto hawa katika kaunti nzima ya Nyamira tena kamati hiyo itakuwa inashughulikia kuambia serikali kama kuna ukosefu wa madarasa na kila kitu ambacho kinahuska katika elimu ya ECD ili serikali iwe inashughulikia kikamilifu,”alisema Rechael Okong’o.
Wakati huo huo, mkurugenzi huyo alisema changamoto watoto hao hupitia wakati wako shuleni haswa katika sekta hiyo ya ECD ni ukosefu wa walimu ambao watakuwa wanatoa mafunzo na ukosefu wa chakula.
“Naomba Jamii ya mkisii iweze kuunga mkono walimu wa ECD ili waweze kutoa mafunzo kikamilifu na tuko na mikakati ya kutengenezea watoto wachanga uji kila siku ikifika 10:00am ili tuweze kuwalinda watoto wetu kikamilifu,” aliongeza Okong’o.