Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kisii Mary Otara amempongeza kamishna wa kaunti hiyo Chege Mwangi kwa kuvunjilia mbali kamati za usalama katika eneo bunge la Bochari.
Kamati hizo za usalama zilivunjwa kufuatia ukosefu wa kutekeleza shughuli zao za kiusalama kikamilifu.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, Otara alisema hatua ya kamishna ni ya kufurahisha kwa kuwa inaonyesha uwazi kwa wakazi wa kaunti ya Kisii.
Wakazi wa Bochari wamekuwa wakiandamana hadi ofisi za kamishna katika siku za hivi majuzi kulalamikia ukosefu wa usalama katika eneo hilo jambo lilomsababisha kamishna huyo kuchukua hatua hiyo ya kuvunja kamati hizo.
Aidha, Otara ameomba maafisa wa polisi kuharakisha kufanya uchunguzi kubaini ni nani aliyehusika kwa kumshambulia naibu chifu wa eneo la Bochari huku ikidaiwa kuwa ni wanachama wa ‘community policing’ walitekeleza mashambulizi hayo.
“Naomba maafisa wa polisi kuharakisha uchunguzi kubaini nani alihusika katika mashambulizi dhidi ya naibu wa chifu katika eneo la Bochari ili wachukuliwe hatua ya kisheria, iwe funzo kwa wananchi wengine,” alisema Otara.