Share news tips with us here at Hivisasa

Baada ya mwanafunzi mmoja kujipata kituoni Ijumaa, Naibu wa Kamishna wa Kaunti ya Kisii Philip Soi amewataka walimu na wazazi kuwajibikia watoto wao wakati maonyesho ya kilimo yanaendelea.

Naibu kamishna huyo alikuwa akiongea siku ya Ijumaa katika Uga wa mchezo wa Gusii ambako aliwatahadharisha wanafunzi dhidi ya kuzurura usiku baada ya maonyesho huku akisema wengine ni wageni katika mazingira ya mjini huku akitaja mojawapo ya kisa cha siku ya Ijumaa ambapo mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi alipotea na kuja kutafuta msaada katika Kituo cha Polisi cha Central mjini Kisii.

Aliongeza kuwa walimu ndio wana wajibu wa kuwachunga watoto hasa wale wa shule za msingi ambao wamekuwa wakiepa wenzao na kuenda mitaani kutembea bila ufahamu wa wasimamizi wao au walimu waliowaleta katika maonyesho.

"Kila mzazi au mwalimu ambaye aliwajibishwa na watoto au wanafunzi sharti ahakikishe kuwa watoto hao wapo salama na sharti wawe pamoja," alisema Soi.

Soi pia aliwahakikishia waliohudhuria maonyesho hayo ya kilimo na biashara kuwa usalama umeimarishwa na vyombo vya usalama vipo wakati wote kwa ajili hiyo akiwataka waweke wasiwasi mbali.

Maonyesho hayo ya kilimo na biashara ambayo yalianza siku ya Alhamisi yanatarajiwa kufika ukingoni siku ya Jumapili ambapo wakazi, haswa wafanyibiashara na wanaoendesha bodaboda wamethibitisha kufaidi pakubwa kutokana na maonyesho hayo.