Usimamizi wa kampuni ya usagaji chai ya Kipkebe kwa mara nyingine tena imezisimamisha kampuni mbili za uuzaji chai kupeleka mazao yao kwenye kampuni hiyo kwa madai kuwa kampuni hizo zinachochea vurugu miongoni mwa wakulima.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Usimamizi wa kampuni hiyo tayari umesimamisha kampuni ya Enchoro na ile ya Nyamiranga kuuza chai yao kwenye kampuni hiyo kufuatia kuafikiwa maamuzi ya uchunguzi wa mwezi mmoja uliofanywa na maafisa wakuu wa kampuni hiyo.

Akizungumzia swala hilo mapema Jumapili, afisa wa ukulima wa nyanjani kwenye kampuni hiyo ya Kipkebe Victor Osugo alisema kuwa vurugu zinazosababishwa  na kampuni zinazouzia usimamizi wa Kipkebe chai ulikuwa unaiharibia jina kampuni hiyo. 

"Tumekuwa tukifanya uchunguzi kuhusiana na swala hilo kufuatia wafanyikazi wa kampuni hizo mbili kupigana hadharani  na tukaamua kusitisha biashara zozote na kampuni hizo mbili kwa mwaka mmoja kwa kuwa kampuni yetu inashtumu vurugu zinazoonyesha picha mbaya kwa kampuni yetu," alisema Osugo. 

Osugo aliongeza kwa kusema kuwa kamwe kampuni hizo mbili hazitaruhusiwa kukata rufaa kuhusiana na uamuzi huo kwa kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha wa kuzihuzisha kampuni hizo na vurugu. 

"Tunashukuru idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kupeana ushahidi mbele yetu, na sio kwamba twazionea kampuni ila hivyo ndivyo hali ilivyo, na kwa maana hiyo, kamwe wahusika hawataruhusiwa kukata rufaa kuhusiana na uamuzi huo," alisisitiza Osugo. 

Aidha, mwenyekiti wa muungano wa chama cha wauza chai cha Nyamiranga Cleophas Abuga alishtumu maamuzi hayo akisema kwamba kwenye vurugu hizo zilizoanzishwa na mahasimu wao wa Enchoro, wafanyikazi wao watano walipata majeraha huku akihaidi kutumia njia mbadala kuhakikisha kuwa biashara zao na kampuni ya Kipkebe hazisitishwi.

"Maamuzi yaliyofanywa kustisha uuzaji wetu chai kwenda Kipkebe haukutupa nafasi ya kujieleza kwa kuwa hata baada ya vurugu kuanzishwa  na mahasimu wetu wa Enchoro, ni wafanyikazi wetu watano waliopata majeraha makali hata hivyo tutatafuta njia ya kuhakikisha kuwa biashara zetu na Kipkebe haziathiriki," alisema Abuga. 

Hali kama hiyo ilikuwa imejiri baada ya kampuni hiyo ya Kipkebe kusimamisha kampuni ya Nyakerinya  na ile ya Chabumba kuwauzia chai kwa miaka miwili mwezi Agosti mwaka huu baada ya kampuni hizo kuhusika kwenye vurugu sawia na hizo.