Afisa wa elimu katika Kaunti ya Kisii amesema serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati kabambe ya kuhakiksha sekta ya elimu katika vyuo vya kiufundi pamoja na shule za chekechea imeinuliwa kikamilifu.
Kulingana na afisa huyo, serikali ya kaunti itajenga majengo mapya katika shule ambazo hazina majengo ya kutosha na kuweka mazingira yaliyo mema kwa elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu afisini mwake iliyoko mjini Kisii, David Kebiro alisema wamekuwa waikipitia changamoto nyingi tangu sekta hizo ziwe chini ya uongozi wa kaunti lakini kufikia sasa, wamejitayarisha kuimarisha sekta hizo.
“Unapoanza jambo fulani, lazima upitie changamoto fulani. Tangu vyuo vya kiufundi na shule za chekechea kuwekwa nchini ya uongozi wa kaunti, tumekuwa na changamoto nyingi lakini sasa tutaimarisha sekta hizo kikamilifu,” alisema Kebiro.
Kebiro aliomba walimu wa vyuo vya kiufundi kufuata utaratibu wa kuajiriwa na kulipwa mishahara wala sio kuandamana.
Walimu wa vyuo vya kiufundi Kisii waliandamana siku ya Jumatatu kulalamikia kutolipwa mishahara yao na kutoajiriwa na serikali ya kaunti hiyo, jambo ambalo afisa huyo alisema litashugulikiwa kikamilifu.