Kaunti ya Uasin Gishu inapania kujenga masoko ya kisasa katika kila mtaa mjini Eldoret ili kupunguza msongamano wa wachuuzi mjini humo.
Masoko hayo yatajengwa katika mitaa ambayo ina idadi kubwa ya watu kama vile mtaa wa Langas, Mnyaka, Kamukunji, Huruma miongoni mwa mitaa mingine.
Mbali na masoko hayo, utawala wa kaunti hiyo unapanga kutenga ardhi zaidi katika kila wadi kwa ujenzi wa masoko.
Akizungumza ofisini mwake siku ya Ijumaa, Naibu Gavana wa Kaunti ya Uasin Gishu Bw Daniel Chemno alisema serikali yake inatambua mchango wa wachuuzi katika mapato ya kaunti, ndiposa utawala huo unafanya kila juhudi ili kuwekea wachuuzi mazingira murua ya kuendeleza biashara yao.
“Tuko na mipango ya kujenga masoko zaidi kwa wachuuzi ili kupunguza msongamano katikakati mwa mji. Wachuuzi wote wanapaswa kuwa tayari kuhamia katika masoko hayo kwa mujibu wa sheria ya kaunti. Wale ambao watapuuza sheria husika hawataruhusiwa kuendeleza biashara yao katikati mwa mji,” alisema Chemno.
Chemno alisema mswada wa bunge la kaunti hiyo kuhusu uchuuzi unalenga kuleta ustaarabu katika sekta ya uchuuzi.
Kiongozi huyo alisema kupitishwa kwa mswada huo na kuwa sheria kutakabiliana na wahalifu ambao hutumia uchuuzi kuendeleza uhalifu mjini humo.
“Mswada huu utatusaidia kama kaunti kutambua wachuuzi halali na kukabiliana na wachuuzi bandia ambao hutumia uchuuzi kuendeleza uhalifu mjini,” alisema Chemno.
Chemno alitaka wachuuzi kujiunga katika makundi na kuanzisha vyama vya ushirika ili kuboresha maisha yao.