Gavana wa Garissa Nathif Jama ameahidi kuwa serikali yake itatumia shilingi milioni 200 ili kuimarisha hali ya usalama katika chuo kikuu cha Garissa.

Share news tips with us here at Hivisasa

Chuo hicho kingali kimefungwa kufuatia shambulizi la kigaidi lililowauwa watu wasiopungua 147, wengi wakiwa wanafunzi mnamo tarehe Aprili 2 mwaka huu, na Jama pamoja na viongozi wengine wa eneo hilo wamekuwa wakishinikiza ufunguzi wake.

Katika hatua ambayo inaonekana kupiga jeki harakati za ufunguzi wake, fedha hizo zinalengwa kutumika katika uboreshaji wa usalama chuoni humo, na pia kujenga sehemu za kutorokea kwa wanafunzi na wafanyikazi endapo shambulizi litatokea.

Jama alihimiza serikali kuu na wizara ya elimu kuharakisha kukifungua chuo hicho kwa kuwa ndicho fahari ya elimu katika eneo hilo.

“Wizara ya elimu na serikali kuu zinapaswa kuharakisha kukifungua chuo cha Garissa ambacho ni fahari yetu kwenye eneo hili,” alisema Jama.

Mwakilishi wa wanawake Halima Ware pia aliisihi serikali kukifungua chuo hicho ili kuwasaidia wanafunzi wanaotaka kujiunga nacho.

Walikuwa wakizungumza siku ya Jumanne wakati wa kongamano la amani chuoni humo la siku nne.