Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia visa vya watoto pamoja na watu wazima kutumbukia kwenye mabwawa ya umma na yale ya kampuni za kibinafsi na kupoteza maisha, serikali ya Kaunti ya Mombasa imetakiwa kuweka vikingi na nyua za kuzuia maeneo kama hayo kufikiwa kiholela na umma.

Akizungumza siku ya Jumatano, katika eneo la Mtongwe kwenye hafla inayoendelea ya kuhamasisha jamii dhidi ya usalama wao nyakati za dharura, mtaalam wa masuala ya baharini Idris Juma, alisema mbinu hiyo itaepusha watu kuingia kwenye vidimbwi, mito, mabwawa pamoja na sehemu za maji ya bahari kiholela, ambapo mara kadhaa kumeshuhudiwa watu kupoteza maisha kwa kujaribu kuogelea kwenye maeneo ya maji mengi.

Mtaalam huyo, alizishauri kaunti zote ambazo zimezingirwa na maji makuu ya bahari na zile zilizo na mito na mabwawa yenye kima kirefu cha maji kuweka usalama kwa kuunda ua na pia kuajiri watu wa kuweka usalama na kuongoza umma katika maeneo husika.

"Hii itakuwa mbinu moja ya kudhibiti maeneo yaliyo na maji kama bahari kwa kuweka nyua pamoja na vijana wa kutoa usalama na mwongozo kwa umma. Kwa kutekeleza hayo, itakuwa rahisi kuzuia maafa ya watu katika bahari na mabwawa,” alisema Juma.