Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Afisa mkuu wa kampuni ya Cyber School Technology Solutions Palas Chanda amesema walimu wote wanafaa kuingia darasani wakiwa wamehamasishwa ili shughuli ya kutoa mafunzo iwe yenye mafanikio.

Akizungumza siku ya Jumatano alipomtembela Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua afisini mwaka, Chanda alisema kampuni hiyo itaanzisha mradi wa kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao ambao unalenga shule 20 hadi 30 kwenye kaunti hiyo.

“Tunataka walimu wote waende darasani wakiwa wamehamasishwa zaidi ili utoaji wa mafunzo ufanikiwa pakubwa. Kutakuwa na ongezeko la wanafunzi na isitoshe, matokeo yatakuwa bora zaidi katika masomo muhimu,” alisema Chanda.

Gavana Mbugua kwa upande wake alisema ingawa elimu haijagatuliwa kabisa, mradi huo ni muhimu katika kubadili dhana ya wanafunzi kuhusiana na masomo ya sayansi na hesabu.

“Nina uhakika mradi huu utasaidia pakubwa katika kuimarisha viwango vya elimu katika kaunti ya Nakuru. Tuko tayari kufanya kazi na mashirika yaliyo na mradi sawia,” alisema Mbugua.

Inaarifiwa kuwa mradi huu utaleta utofauti katika kutoa mafunzo na katika kujifunza masomo ya sayansi na hesabu shuleni.

Kampuni hiyo hutumia mtandao katika kutoa mafunzo ya masomo ya sayansi na hesabu na kufikia sasa, imeanzisha mradi huo katika shule 80 hapa Kenya.