Kijana mmoja amehukumiwa kifungo cha miaka mine gerezani na mahakama moja ya Nakuru siku ya Ijumaa baada ya kukubali shtaka la wizi wa simu za rununu pamoja na pesa.
Mshtakiwa, Maxwell Omondi, alifikishwa mahakamani kwa kosa la wizi wa Sh50,000 na simu aina ya Techno yenye thamani ya Sh4,000 kutoka kwa Hellen Wairimu mnamo tarehe Septemba 30, 2015 mjini Nakuru.
Upande wa mashtaka uliarifu mahakama kuwa Omondi alielekea hadi katika afisi ya mlalamishi na kufungua droo ambapo pesa hizo na simu zilikuwa na kisha kuziiba.
Omondi pia alikabiliwa na shtaka mbadala la wizi wa simu ya rununu aina ya Samsung Galaxy yenye thamani ya Sh8,560 kutoka kwa Abdi Omar mnamo tarehe Septemba 24 katika eneo la YMCA viungani mwa mji wa Nakuru.
Upande wa mashtaka uliarifu mahakama kuwa Omondi aliomba simu hiyo kutoka kwa mlalamishi kwa madai kuwa alikuwa anataka kupiga simu kabla ya kutoweka.
Pamoja na hayo, alikabiliwa na shtaka la tatu la kuiba simu ya rununu aina ya Techno yenye thamani ya Sh2,500 kutoka kwa Shafi Alisudra mnamo tarehe Septemba 24 katika eneo la Section 58 viungani mwa mji wa Nakuru.
Licha ya mshtakiwa huyo kukubali mashtaka hayo mbele ya Hakimu mkuu wa Nakuru Liz Gicheha na kuomba mahakama imwonee huruma, upande wa mashtaka uliomba aadhibiwe ukisema kwamba uchunguzi wa polisi umebaini kwamba mshtakiwa amepatikana na makosa ya uhalifu mara kwa mara.
Mahakama hiyo ya Nakuru ilimhukumu kifungo cha miaka miwili kwa kila kosa huku ikiagiza vifungo hivyo vifuatane.
Walalamishi waliripoti matukio hayo kwa maafisa wa polisi na Omondi alikamatwa tarehe Oktoba 11 mjini Nakuru na hapo akapelekwa katika Kituo cha polisi cha Central huko Nakuru.