Kiongozi wa kundi la majambazi la ‘Raia’ anayedaiwa kufadhili kundi hilo kuendeleza uovu alitiwa mbaroni katika eneo la Kinoo.
Akizungumza siku ya Ijumaa, mkuu wa police katika eneo la Kikuyu, Mutune Maweu alisema kwamba mshukiwa huyo alitiwa mbaroni katika nyumba yake katika mtaa wa Kinoo.
Alieleza kwamba polisi wa eneo la Kinoo walimkamata na waliweza kupata bunduki sita na risasi thelathini ikiwemo bidhaa zingine za thamani.
Maweu alisema kwamba polisi wa kituo cha kinoo waliweza kupewa ripoti na mkaazi wa eneo hilo aliposhuku mienendo yake.
Alieleza kwamba polisi walienda hadi nyumbani kwake masaa ya asubuhi na kumpata akiwa amelala.
Mkuu wa polisi alieleza kwamba waliweza kunasa bidhaa za thamani zilizokuwa zimewekwa kwenye sanduku chini ya Kitanda.
Alitaja vifaa kama simu za bei ghali, saa sita za dhahabu zinazodaiwa kuibiwa katika duka fulani eneo la Westlands, na pesa taslimu laki nane.
Maweu alieleza kwamba mshukiwa huyo amekuwa akisakwa na maafisa wa polisi katika eneo hilo kwa madai kwamba anafadhili kundi hilo kwa bunduki, na pia mbinu mbali mbali za kiujambazi.
Alieleza kwamba mshukiwa huyo anadaiwa kumuua mwanadada mmoja katika eneo la Kabete mwaka jana.
"Mshukiwa amesakwa kwa muda mrefu na kushikwa kwake ni kwa manufaa sana kwa ajili amekuwa akiwaingiza vijana wadogo katika ujambazi wa hali ya hatari. Nawashukuru wakaazi ambao waliweza kuripoti mshukiwa huyu kwa kuwa wanajali usalama wao.Nawahisi wakaazi wote waige mfano huo na kuripoti mtu yeyote wanaomshuku," alisema Maweu.
Teresia Mwai, mkaazi wa eneo hilo alisema kwamba hakujua kwamba jambazi huyo sugu aliishi hapo.
Alifichua kwamba jambazi huyo alikuwa mpole na mwenye heshima kwa akina mama.