Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira Alice Chae ameiomba tume ya mitihani nchini kukomesha visa vya wanafunzi kushiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

Hii ni baada ya kusemekana kuwa viwango vya wizi wa mitihani vimeongezeka kwa asilimia kubwa nchini.

Akizungumza siku ya Jumapili katika Kanisa la Great Miracle lililoko eneo la Mobamba, mwakilishi huyo aliiomba tume ya KNEC kujaribu kila iwezalo kukomesha wizi wa mitihani kwa kusema kuwa huenda matokeo ya mitihani kwa wanafunzi wa mwaka huu yasiwafaidi katika siku sijazo.

Wakati huo huo, Chae alisema tume ya KNEC imekuwa ikiheshimika kwa miaka mingi iliyopita kwa kuaminiwa na watu wengi lakini isipokomesha na kuziba wizi wa mitihani unaoendelea kushuhudiwa nchini, basi mitihani ya tume hiyo huenda isiaminiwe kamwe.

“Naomba tume ya mitihani nchini KNEC kuweka mikakati mwafaka ili visa vya wizi wa mitihani vipungue na visishuhudiwe tena nchini, maana huenda tume hiyo isiaminiwe nchini na kusababishia wanafunzi wetu hasara kwa masomo yao wanapoenda kutafuta ajira,” alisema Chae.

Hata hivyo aliomba wanafunzi ambao wanaendelea kufanya mitihani kuendelea kujitenga na wizi huo ili kupata matokeo mema majibu yatakapotangwazwa mwaka ujao.