Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Askofu wa dayosisi ya Eldoret ya kanisa la katoliki Cornelius Korir amekosoa baadhi ya makundi ambayo yanaendeleza juhudi za kuhubiri amani katika maeneo ya North-Rift kwa kupuuza wazee.

Askofu Korir alisema wazee walichangia pakubwa katika juhudi za kuhubiri amani na upatanisho wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008, lakini kwa sasa wametemwa.

Akihutubu katika dayosisi ya kanisa la katoliki mjini Eldoret baada ya kufanya kikao na wazee  hapo Jumatatu kutoka katika kaunti sita za North-Rift, askofu Korir alionya kwamba iwapo wazee wataendelea kupuuzwa, itakuwa vigumu kupatanisha jamii za eneo hilo.

Korir aliwataka wahasisi wa mikutano ya maombi kwa wahasiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu, na naibu rais William Ruto pamoja na mwanahabari Joshua Sang kuzingatia mawaidha ya wazee kuhusu maombi hayo.

"Ukiangalia watu ambao wanadai kuongoza maombi haya utashangaa walikuwa wapi wakati wazee walikuwa wakitumia kila mbinu kupatanisha Wakenya wakati wa ghasia za 2007/2008," alisema Korir.

"Itakuwa vizuri sana iwapo tutaendelea kutambua mchango wa wazee hawa kwa kuwahusisha katika maswala ya kuhubiri amani pamoja na kufanyia maombezi kwa naibu rais William Ruto na mtangazaji Joshua Sang," aliongezea.

Askofu Korir alionya dhidi ya watu ambao wameanza kudai kuwa wana ushahidi kuhusu njama ya kuhonga mashahidi ili kufanya njama ya kutoa ushahidi wa uongo.

“Hawa watu walikuwa wapi wakati kesi hii ilianza, mbona watokee sasa na kuanza kudai kuwa walikuwa wakihonga mashahidi, huu si wakati muafaka wa kutoa madai hayo,” alisema askofu Korir