Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Mombasa wamepinga vikali hatua ya Halmashauri ya Bandari ya Mombasa (KPA) inayolenga kuwasimamisha kazi zaidi ya wafanyikazi elfu nne.

Wakizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumanne, viongozi hao wakiongozwa na Mbunge wa Nyali Hezron Awiti walisema kwamba hatua hiyo itachangia ongezeko la visa vya kihalifu mjini Mombasa kutokana na idadi kubwa ya vijana kukosa ajira.

Awiti alisema kwamba hatua ya halmashauri za serikali kuwasimamisha kazi vijana wadogo inachangia hali ngumu ya maisha pamoja na kukithiri kwa visa vya kihalifu miongoni mwa jamii,  na akasema kwamba yanayopangwa kufanya na KPA hayafai kwa sasa.

“Hatua ambayo KPA inataka kuchukuwa kwa sasa itachangia hali ngumu ya maisha na kusababisha kukithiri kwa visa vya kihalifu kutokana na idadi kuwa ya watu kukosa ajira, na sisi kama viongozi hilo hatutakubaliana nalo. Tunataka KPA iwatengee sehemu zengine watu wetu wafanye kazi,” alisema Awiti.

Aidha, alipendekeza idadi hiyo ya watu wanaolengwa kusimamishwa kazi kupelekwa katika eneo jipya la kuegesha meli linalotarajiwa kukamilika kufikia mwaka ujao ili kuzuia hali ngumu ya maisha kwa wakenya.

“Kuna eneo jipya KPA inatengeza, sehemu ya kuegesha meli, hawa watu wapelekwe huko wafanye kazi badala ya kuwasimamisha kwa kisingizio cha kukosa pesa za kumudu gharama ya kuwalipa ilhali KPA inatengeza mamilioni ya pesa kila mwezi,” aliongeza Awiti.

Hata hivyo, aliushutumu mrengo wa Jubilee kwa kushindwa kutekeleza ahadi walizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi uliyopita, na akamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuweka mikakati mwafaka ya kubuni ajiri kwa vijana na kusitisha umaskini.