Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu wa chifu wa kata ndogo ya Seregeya eneo la Turbo amewataka wakaazi wa eneo lake kuishi kwa umoja kama njia moja ya kuimarisha usalama eneo hilo.

Diana Owano aliyasema haya alipowahutubia waombolezaji kwenye hafla ya matanga katika kijiji cha Chepkoilel siku ya Jumatatu, na kusema kuwa iwapo wakaazi hawataishi kama ndugu, basi maafa mengi huenda yakatokea yakiwemo ujambazi na wizi.

Owano aliongeza kuwa mpango wa nyumba kumi ulioanzishwa na serikali ya kitaifa ulikuwa ni wa manufaa ya mwananchi wa kawaida kwa kuzingatia usalama kwenye kiwango cha chini namna hiyo.

“Serikali imefanya vizuri kuanzisha mpango wa nyumba kumi na nataka niwahakikishie kuwa kata yetu lazima izingatie agizo la serikali,” alisema Owano.

Aidha, Owano amewataka wakaazi kuwa macho na kuripoti kisa chochote kinachoweza kuhatarisha maisha yao kwa maafisa wa usalama ili hatua madhubuti ichukuliwe.

Pia, amewataka wazazi kujukumika ili kuona kuwa uraibu wa mihadarati kwa vijana wa umri mdogo unakomeshwa, na kuwaamuru wazazi wote kuwarudisha shuleni watoto walioacha masomo yao pindi tu shule zitakapofunguliwa mwezi Septemba.

“Kwa kufanya hivi, tutakuwa tunaendeleza eneo letu kiuchumi na kimasomo na ndivyo tutakapoimarika Zaidi,” alisema.

Owano amewasuta viongozi wote ambao wanatumia nafasi zao kujinufaisha wao wenyewe na familia zao, huku wananchi wakibakia kwenye lindi la umaskini, akisema ni sharti vilio vya wananchi vipewe kipaumbele ili kustawisha eneo hilo na nchi ya Kenya kwa ujumla.