Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Maafisa wawili wa kaunti ya Kisii waliosimamishwa kazi na spika wa kaunti hiyo wamedinda kujiondoa kazini, huku wakisema kuwa kuwa sheria haikufuatwa wakati wa kupokezwa barua za kuwataka kujiondoa kazini.

Maafisa hao, James Nyaoga, ambaye ni karani wa bunge la kaunti pamoja na msimamizi wa kitengo cha fedha katika bunge la kaunti walipokezwa barua za kuwataka kujiondoa kazini siku ya Ijumaa na spika Kerosi Ondieki, kufuatia zogo lililoshuhudiwa hivi majuzi kati ya ofisi za maafisa hao wawili na wawakilishi wa wadi ambao walikuwa wakilalamikia kutolipwa marupurupu yao, ambako wawakilishi hao wadi walizifunga afisi husika.

Kupitia ujumbe kwa vyombo vya habari siku ya Ijumaa, Nyaoga alisema kuwa utaratibu ulitumiwa kuwasimamisha ulikuwa kinyume na sharia, na kuongeza kuwa hela ambazo zilikuwa zikidaiwa na wawakilishi hao hazikuwa za halali na kuwataka wakati wote kufuata sheria wanapowasilisha lalama zao.

Naye msimamizi wa pesa Bwana Amenya aliwashauri wawakilishi wadi hao ambao walikuwa wakizua fujo kati kati ya wiki kuwa na njia mwafaka ambayo inakubalika kisheria, kuliko kutumia njia mkato kutaka kulipwa hela ambazo hawastahili.

Aliongezea kuwa huenda wakaenda kortini kupinga kusimamishwa kwao na spika wa kaunti hiyo.

Mzozo ulizuka siku ya Jumatano ambapo wawakilishi wa kaunti hiyo ya Kisii waliandamana hadi afisi ya karani pamoja na msimamizi wa pesa katika kaunti hiyo wakitaka kulipwa pesa za baadhi ya vikao, kabla ya kuzifunga afisi za maafisa hao, suala ambalo huenda likazua mgongano kati ya wawakilishi na afisi husika tatu ikijumuisha ile ya spika na ya maafisa hao wawili.