Wakaazi wa eneo la Ogembo wamewashtumu maafisa wa polisi waliofika katika eneo hilo hiyo jana, Jumapili wakati ajali mbaya ilipotokea kwa kukosa kuweka usalama katika eneo hilo.
Wakiongea hii leo, Jumatatu na waandishi wa habari katika eneo hilo la ajali, wakaazi hao walisema kuwa maafisa wa usalama waliofika katika eneo hilo la mkasa walikosa kuweka usalama wa kutosha, na wangezuia ajali ya pili ambayo ilitokea katika eneo hilo iliyowahusisha watazamaji waliokuwa wakishuhudia mkasa huo.
Kulingana na wakaazi hao, maafisa hao wangeweka usalama wakati ajali ya kwanza ilipotokea na kufunga barabara hiyo kwa mda, na walifanya hivyo wakitumia mawe, lakini baadaye wakaondoa mawe hayo kabla ya gari la pili kuwagonga watu wawili na wakafa papo hapo.
“Wakati ajali ya kwanza ilifanyika, wakaazi walifika hapo na kufunga barabara ili isiwe inatumika kwa mda, lakini wakati polisi walikuja wakatoa mawe hayo ndiposa gari la pili likakuja bila kujua na kuwauwa watu wawili tena,” alisema David Nyaguta mkaazi.
Kwa sasa, wamewaomba maafisa wa usalama kuwajibika wakati mkasa unapotokea ili kuzuia maafa mengine zaidi kama yale yaliyoshuhudiwa hiyo jana.
Kwingineko, wameomba wenzao wakati ajali imetokea wasiwe na nia ya kuwaibia waathiriwa licha ya kuwasaidia kama ilivyoshudiwa hapo jana.