Maafisa wa polisi wilayani Borabu, kaunti ya Nyamira waliwazuia ng’ombe zaidi ya 20 ambao inasemekana waliibwa kutoka eneo hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika eneo la Borabu, mkuu wa polisi wa kituo cha polisi cha Sotik Timothy Nduale alisema ng’ombe hao walifumaniwa wakiwa katika zizi usiku wa kuamkia Jumanne kwa mkaazi mmoja wa eneo la Manareti Borabu, baada ya kupokezwa habari kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo

Maafisa wa polisi wa kituo cha Borabu wamewaomba wananchi ambao waliibiwa ng’ombe kutoka sehemu mbalimbali za Kaunti ya Nyamira, Nakuru na Bomet kuenda hadi eneo la Memisi kaunti ya Nyamira ili kuwatambua ng’ombe hao.

Kwa upande mwingine, wakaazi wa eneo hilo walilalamikia hali hiyo, na kuomba maafisa wa polisi kuwahakikisha usalama wa kutosha ili wasiendelee kukabiliwa na hasara hiyo.

“Sisi kama wakaazi wa eneo hili la Manga hadi eneo la Borabu tunaomba vituo vya polisi kuongezwa katika eneo hili ili wizi usiwe unashuhudiwa kila kuchao,” alisema Erick Omwanza, mkaazi.

“Kwa maoni yangu, tukiwekewa usalama wa kutosha na maafisa wa polisi wawe wakizunguka hapa nyakati za usiku, wezi hao hawatakuwa katika sehemu hizi kamwe,” alidokeza Peter Bosire, Mkaazi mwingine

“Tukihakikishiwa usalama hatutakuwa na kilio cha kuibiwa ng’ombe wetu serikali itukumbuke kama wananchi wa kawaida,” alisema Meshack Osoro, mkaazi mwingine.