Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi ameapa kushirikiana na kufanya kazi pamoja na Gavana James Ongwae ili kufanya maendeleo zaidi katika kaunti hiyo.

Hii ni baada ya kusemekana kuwa wawili hao wamekuwa wakitofautiana kidogo jambo ambalo limekuwa likikzua mdahalo mkubwa miongoni mwa viongozi pamoja na wananchi wa kaunti hiyo kwa kuhofia kutofanyiwa maendeleo kikamilifu.

Akizungumza siku ya Jumatano katika taasisi ya mafunzo ya wakulima iliyoko viungani mwa mji wa Kisii, wakati wakulima na washikadau katika sekta ya kilimo na ufugaji walikuwa wanawaeleza wakulima jinsi ya kufanya kilimo kiteknolojia, Maangi aliwahakikishia wananchi wa kaunti hiyo kuwa atafafanya kazi pamoja na Gavana Ongwae ili kuhakikisha kaunti hiyo inasonga mbele kimaendeleo.

Aidha, Maangi alimhakikishia Gavana Ongwae kuwa wale wanaowatenganisha wanapoteza muda wao kwani walichaguliwa kufanya kazi pamoja ili kunufaisha watu wa kaunti hiyo kimaendeleo.

“Mimi na Gavana Ongwae tutafanya kazi hadi mwaka wa 2017 kama njia mojawapo ya kutimiza yale tuliyowaahidi wananchi wakati tulikuwa kwa kampeini, Sharti tuyatimize kabla ya uchaguzi ujao,” alisema Maangi.

Maangi pia aliomba magavana wote nchini kufanya kazi na manaibu wao pamoja na kusema kuwa ikiwa wawili hao hawatafanya kazi pamoja, basi hakutakuwa na maendeleo nchini hasa sehemu za mashinani.

Matamshi ya Maangi yaliungwa mkono na Gavana Ongwae aliyekuwa kwa hafla hiyo ambaye alisema watahakikisha maendeleo yamefanywa zaidi kwa wananchi wa kaunti ya Kisii.