Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amesema yeyote atakayepatikana akivuja pesa za wananchi atatiwa mbaroni na kushtakiwa.
Hii ni baada ya madai kubaini kuwa baadhi ya wafanyikazi katika serikali ya kaunti ya Kisii walivuja pesa ambazo wananchi wanatozwa ushuru.
Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari katika mji wa Kisii, Naibu Gavana Maangi alisema kuwa wao kama serikali ya kaunti lazima walinde haki za mtozwa ushuru kwa kufanya maendeleo kwani wao ndio hutoa pesa hizo.
“Nataka niwahakikishie wananchi kuwa pesa zao zitalindwa kikamilifu na serikali ya kaunti yetu. Pesa hizo zitaheshimiwa kikamilifu na kufanya kazi ya maendeleo. Yeyote atakayepatikana akivuja pesa za mwananchi atakabiliwa kisheria kwani ni njia mojawapo ya kukiuka haki za mtozwa ushuru,” alisema Maangi.
Wakati huo huo, naibu gavana alikiri kuwa pesa za kaunti hiyo hazijatumika vibaya. Hii ni baada ya mfanyi hesabu wa pesa katika kila kaunti humu nchini kutoa ripoti kuwa kaunti ya Kisii ilitumia pesa vibaya ambapo alidai shilingi millioni 278 zilikabidhiwa maafisa wa kaunti ya Kisii kinyume na sheria, madai ambayo naibu gavana Maangi alikanusha.
“Yeyote akabidhiwaye mkopo wa serikali katika serikali ya kaunti yetu mshahara wake ndio hugharamia mkopo huo lakini hayo mengine ya kusema kuwa serikali ilitumia pesa vibaya ni uongo mtupu,” alisema Maangi.