Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amewaomba wazee wote nchini kuombea nchi ya Kenya ili kuwe na amani na maendeleo.
Maangi alisema kuwa wazee wakiwa na imani na kujitolea kuombea nchi, basi taifa halitakuwa na changamoto zozote hasa zile zinaendelea kuikumba nchi ya Kenya.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika Chuo Kikuu cha Kisii wakati wa mkutano wa baraza la wazee (National Elders Conference) ulioandaliwa katika chuo hicho na kuwaleta pamoja wawakilishi wote wa baraza kutoka kaunti 47 za nchi, Maangi aliomba maombi ya kipekee kutoka kwa wazee ili Kenya iwe na amani na maendeleo.
Wakati huo huo, Maangi pia aliwaomba wananchi kuombea viongozi ili wawe na maarifa ya kuongoza taifa.
Alisema kuwa hatua hiyo itafanya nchi iinuke kimaendeleo na kiuchumi na liwe miongoni mwa mataifa ambayo yatakuwa ya kwanza kwa maendeleo barani Afrika Mashariki.
“Hakuna taifa ambalo litaendelea kama haliombewi na kuwa na amani. Naomba nchi ya Kenya iwekwe kwa maombi ili iwe na amani,” alisema Maangi.
Aliongeza: “Amani huanza na wewe pamoja na mimi. Tushikane mikono tuombee amani, serikali na viongozi ili nchi yetu iweze kusonga mbele.”