Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi amewaomba walimu kutia motisha katika masomo ili wanafunzi waweze kupita katika mitihani ya Kitaifa.

Hii ni baada ya walimu hao kupata nyongeza yao ya mishahara kwa asilimia kati ya 50-60 jinsi ilivyopendekezwa na mahakama kuu.

Akizungumza siku ya Jumatatu na waandishi wa habari mjini Kisii, baada ya uamuzi huo wa mahakama kutolewa, Maangi alisema walimu wamepata haki ambayo wamekuwa wakifuata kwa muda mrefu.

Alisema kuwa kwa vile kilio chao kimesikika, wanapaswa kutia bidii kwa vile maslahi yao yameshughulikiwa kikamilifu.

Maangi alisema kuwa serikali ya kitaifa inapaswa kushughulikia swala hilo la mishahara ya walimu kikamilifu na kuhakikisha kuwa walimu hao wamepata mishahara hiyo.

“Naomba kila mwalimu sasa awe na motisha ya kuwafunza watoto wetu. Lile tunahitaji kusikia kama viongozi ni kuwa wanafunzi wamefanya vyema katika mitihani kwani upande wenu umetekelezwa na muhakikishe upande wa wanafunzi umetekelezwa vilevile,” alisema Maangi.

Walimu wamekuwa wakigoma kila mara wakidai nyongeza ya mishahara yao kwa asilimia kati ya 50 na 60 lakini hayo yaliweza kutekelezwa jambo ambalo limewafurahisha walimu wote nchini.

Mwenyekiti wa chama cha KNUT nchini Wilson Sossion alisema uwazi umeonyeshwa kwa walimu wote nchini kupitia mahakama na kupongeza uamuzi huo.